28 Novemba 2019 - 07:06
Kuunga mkono tena Marekani machafuko ya Iran; kukariri uadui dhidi ya taifa la Iran

Katika kipindi cha uongozi wa Rais Donald Trump, serikali ya Marekani ikiwa na lengo la kutekeleza siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa, imeiwekea Iran vikwazo vikali zaidi.

(ABNA24.com) Sambamba na hatua hiyo, kuibuka fujo na machafuko hivi karibuni hapa nchini, kuliipa matumaini Marekani kwamba, inaweza kufikia malengo yake haramu kupitia kuwaunga mkono wahuni na wafanya fujo.

Katika kipindi cha majuma matatu ya hivi karibuni, viongozi wa Marekani wamenukuliwa mara chungu nzima wakitangaza dhahiri shahiri kwamba, wanawaunga mkono wafanya fujo na waendesha machafuko hapa nchini. Aidha viongozi hao wamesikika wakitaka jamii ya kimataifa kuwaunga mkono wafanya fujo na wanendesha machafuko nchini Iran.

Akthari ya viongozi wa Marekani akiwemo Rais Donald Trump wametangaza wazi wazi kuwaunga mkono watu walioanzisha fujo na kuzusha ghasia kwa kisingizio cha kulalamikia ongezeko la bei ya petroli hapa nchini.

Msimamo wa hivi karibuni kabisa ni ule uliotangazwa na Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Jumanne ya juzi ya tarehe 26 Novemba, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo aliwahutubu wafanya ghasia hapa nchini alisema: Marekani inasikia kilio na sauti zenu, inakungeni mkono na itaendelea kuwa bega kwa bega na nyinyi.

Kadhalika ameahidi kwamba, Marekani itashadidisha vikwazo dhidi ya Iran mara hii kwa kisingizio cha haki za binadamu. Pompeo amesema kwa mara nyingine tena kwamba, Washington inafanya juhudi ili kuibadilisha Iran na kuifanya iwe "nchi ya kawaida".

Matamshi mapya ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwa hakika ni kukaririwa tena utendaji wa kiadawa na uhasama wa serikali ya Trump dhidi ya Iran na ni sisitizo jingine la ndoto za alinacha za Washington kuhusiana na Iran.

Machafuko na vurugu za hivi karibuni nchini Iran zilizofanyika kwa kisingizio cha kulalamikia ongezeko la bei ya petroli zilianza Ijumaa ya tarehe 15 Novemba.

Kwa mtazamo wa Marekani hiyo ilikuwa fursa ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran na ndio maana Washington haikutosheka tu na kuwaunga mkono wafanya fujo na wazusha machafuko tena wazi na bayana, bali ilifanya juhudi za kushadidisha mashinikizo ikijidanganya kwamba, kwa kufanya hivyo itaweza kufikia malengo yake.

Nyaraka zilizopo zinaonyyesha kuwa, Marekani ilikuwa nyuma ya pazia ya mipango ya kuzusha machafuko hapa nchini na uharibifu wa mali za watu na za umma wakati wa kujiri fujo hizo.

Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa, vurugu na fujo hizo hazikufanywa na watu wa kawaida, bali ni matokeo ya senario iliyokuwa imepangwa na kuandaliwa hapo kabla.

Serikali ya Trump ikiendeleza utendaji wake ulio dhidi ya Iran siyo tu kwamba, imeshajiisha na kuchochea machafuko ya hivi karibuni hapa nchini, bali imetoa wito wa kushadidishwa mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Brian Hook, mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran, huku akitoa madai ya kukaririwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa matamshi ya uingiliaji wa moja kwa moja katika masuala ya ndani ya Iran kwa kusema kuwa, Marekani inaunga mkono kikamilifu ghasia na machafuko hapa nchini.  Hook alinukuliwa hivi karibuni akisema wazi kwamba, Marekani imefurahishwa mno na anga iliyojitokeza nchini Iran.

Kwa mtazamo wa Iran ni kuwa, serikali ya Marekani inataka kutumia vibaya anga iliyojitokeza kwa ajili ya kufikia malengo yake machafu na katu haina nia njema kabisa na wananchi wa Iran.  

Misimamo ya viongozi wa Washington pia, ni maana halisi ya uingiliaji masuala ya ndani ya Iran, hatua ambayo ni kinyume kabisa nasheria kwa mtazamo wa sheria za kimataifa na inakinzana pia na kanuni na misingi ya kimataifa kama ambavyo hatua hizo ni kinyume kabisa na hati ya Umoja wa Mataifa.

...........
340